WEMA AMWAGA CHECHE KWENYE OFISI ZA GLOBAL
HOVYOOO! Wema Isaac Sepetu aliye pia Miss Tanzania 2006, amejitoa fahamu kwa kupandisha mzuka na kutinga makao makuu ya Kampuni ya Global Publishers, Bamaga-Mwenge, Dar na kuzua timbwili la aina yake kisa kikiwa ni kuandikwa kwa habari zake na mpenziwe, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Tukio hilo la kumchoresha staa huyo mwenye vituko kila kukicha,
lilijiri Jumatatu iliyopita kwenye ofisi za Global ambao ni wachapishaji
wa gazeti hili (Amani), Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Championi na
Risasi majira ya mchana kweupe hivyo kufunga mtaa huku wapita njia
wakimzodoa kwa maneno ya kejeli.
ATINGA NA WAPAMBE DHAIFU Akiwa na kundi la wapambe
dhaifu na goigoi wakiongozwa na meneja wake, Martin Kadinda waliosimama
nje ya ofisi hizo, Wema alifika kwa upole akionekana mkarimu kwa mlinzi
ambapo aliomba kuonana na mwandishi nguli wa magazeti pendwa, Imelda
Mtema.
Mlinzi alimruhusu kwa vile Global ni mjengo wa mastaa na watu wasio
mastaa, huwa hawakauki kuingia na kutoka kwa mambo mbalimbali.
Wema alipofika mapokezi, pia aliomba kuonana na mwandishi huyo lakini
tofauti na utaratibu ambapo huwa mgeni akifika huulizwa kama ana
‘apointimenti’ ili aitiwe anayemhitaji, Wema alipitiliza kwa nguvu hadi
chumba cha habari akifuatana na kijana aliyekuwa akimrekodi.
Wema akiwa ndani ya News Room akimtafuta mwandishi wa Global Imelda Mtema, huku akisema yeye ni chizi!
Akiwa ndani ya chumba cha habari, Wema aliuliza kwa sauti ya juu na ya kujiamini: “Imelda yupo wapi? Nauliza Imelda yupo wapi?”
WEMA NA IMELDA Katika kumtafuta Imelda kwa macho kwa
sababu chumba cha habari ni kikubwa huku akionywa na wahariri kwamba
atulize mzuka kisha aeleze shida yake, Wema alimuona Imelda akitoa
maelezo kwa Mhariri Kiongozi wa Magazeti Pendwa ya Global, Oscar Ndauka
kuhusu habari aliyokuwa ameifuatilia.
Cha kushangaza, Wema alimfuata Imelda mpaka kwenye meza ya mhariri huyo kisha kuanza kufoka kwa sauti ya juu.
MSIKIENI WENYEWE “Kwa nini mnafuatilia maisha yangu? Kila siku mnaniandika na Diamond. Kwa nini Imelda unaniandika kuwa mimi msagaji?”
“Mimi ni chizi, nakwambieni mimi ni chizi zaidi ya machizi wote”….Wema alikuwa akifoka mwanamke!
ATULIZWA, AGOMA Katika kuhoji huko, mhariri kiongozi
alijaribu kumtuliza Wema ambaye alikuwa kama amewehuka: ”‘Wema
tuelewane, eleza shida yako kwa utaratibu kwani hakuna ofisi isiyokuwa
na utaratibu.”
Pamoja na kuambiwa hivyo bado Wema aliyekuwa ameshika Gazeti la
Ijumaa Wikienda toleo la Jumatatu iliyopita, aliendelea kumng’ang’ania
Imelda ambaye alikuwa akijaribu kumtuliza:
“Wema twende tukakae pale kwenye meza ya mkutano uwaeleze viongozi
wangu tatizo lako. Hiyo stori kuwa wewe ni msagaji mbona haipo, ni
gazeti gani?”
Licha ya kupewa mwongozo huo, Wema aliendelea kufoka: “Hivi mnajua
mimi ni chizi? Kwa taarifa yenu mimi ni chizi zaidi ya machizi wote,
ohooo!”
MLINZI ATONYWA, ATIA TIMU Baada ya hali kuwa tete,
mlinzi wa geti kuu alipigiwa simu ya mezani na kujulishwa juu ya Wema
kusababisha kazi kusimama ambapo alifika haraka tayari kwa kumtoa nje
kwa hiyari yake au lazima.
Ndipo kukatokea timbwili kubwa, wapambe wake ‘goigoi’ nao waliingia
wakitaka kufanya vurugu ili kumteka mwandishi huyo lakini kikosi imara
cha Global kikiongozwa na Mhariri Kiongozi wa Magazeti ya Championi,
Saleh Ally kilijiimarisha na kutuliza fujo hizo huku kikiwa makini
kuhakikisha Wema na timu yake hawajeruhiwi hata kidogo.
WEMA ATUMIA GAZETI KAMA SILAHA Katika purukushani
hiyo, Wema alionesha udhaifu wa kumudu varangati pale alipotumia gazeti
aliloshika kumpiga nalo mwandishi Imelda, jambo lililodhibitiwa kama
Waasi wa M23 wa Kongo walivyodhibitiwa na Majeshi ya Umoja wa Mataifa,
akatolewa nje.
MBALI NA WEMA Ukiachia mbali Wema kutulizwa kwa
kutolewa nje kwa nguvu, vijana wake walegevu nao waliwekwa chini ya
himaya ya Global kwa kunyang’anywa kamera ya video iliyokuwa ikitumika
kuchukua matukio huku nao wakipigwa picha za kutosha na wapiga picha
wetu.
VITA KUBWA, WEMA AVUA VIATU Nje ya ofisi, ‘vita’
kubwa kati ya Wema na walinzi wa Global (alifika mwingine kutoka lindo
la mbali) ilizuka ambapo staa huyo alivua vile viatu vyake virefu vya
rangi ya bluu bahari na kuanza kumpiga navyo mmoja wa walinzi hao
akiamini anamkomesha lakini pia akadhibitiwa!
Wema
akiwa ameshika viatu vyake vya mchuchumio mkononi baada ya kutolewa nje
ya ofisi na wapambe wake akiwemo meneja wake, Martin Kadinda (kulia).
Wema akiwa anarandaranda kwenye geti kuu akiwa peku, alidondosha
matusi ya nguoni ambayo hayaandikiki gazetini kwa namna yalivyokuwa
makali. Ilikuwa si rahisi kuamini kuwa yeye ni kioo cha jamii.
Timbwili la Wema na wapambe wake akiwemo Petit Man, ambao hawakufua
dafu kwa walinzi na vijana wa Global nje ya ofisi hizo, lilichukua zaidi
ya nusu saa huku likikusanya kadamnasi na kusababisha mtaa kujifunga
wenyewe.
POLISI HAO Hata hivyo, uongozi wa Global
uliwasiliana na Polisi wa Kituo cha Kijitonyama ‘Mabatini’, Dar ambao
walifika na kumkuta Wema na timu yake wakiwa wamepoa mlangoni,
wakaambiwa timbwili limetulia hivyo wakatimua zao.

‘Baby’ wa Diamond Platnumz
alikuwa hashikiki viatu viligeuka kuwa ‘mzigo mzito’ akivibagwa chini
huku akitoa mkwara akiwa pekupeku na kufunga mtaa.
APEWA KAMERA, KADI NOOOO!
Baadaye Wema aliomba kupewa kamera yake ambapo zoezi hilo lilifanyika
lakini ‘memori kadi’ yenye picha walizoanza kurekodi, ilitolewa ili
kupisha maridhiano kwanza. Waliambiwa kadi hiyo ilitolewa kwa sababu
walirekodi bila idhini au kibali cha Kampuni ya Global.
WEMA AGOMA KUONDOKA Baada ya kugundua kadi ya kamera
ipo chini ya ulinzi wa Global, Wema alitaka kulianzisha tena akidai
hawezi kuondoka hadi apewe kadi hiyo lakini uongozi uliweka ngumu.
Baadaye aliondoka kimyakimya. Wakati huo wapambe wake walishaondoka
kitambo.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, kadi ya kamera hiyo bado
ilikuwa inashikiliwa na uongozi wa Global ili kumthibitishia Wema kuwa
hawezi kufanya umafia wowote dhidi ya waandishi wa kampuni hiyo yenye
nguvu kihabari nchini Tanzania.
Comments
Post a Comment