Tuseme yetu, waseme yao kwa Katiba bora.

TUME ya Mabadiliko ya Katiba imetangaza kuanza kwa awamu ya pili ya mchakato wa kukusanya maoni ya Watanzania, kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya ya nchi.
Uamuzi wa tume kutangaza awamu hiyo ya pili unatokana na kukamilika kwa awamu ya kwanza. Katika awamu ya kwanza, tume imezuru mikoa minane Tanzania Bara pamoja na Zanzibar, ambako imekutana na wananchi na kuwasikiliza.
Tathmini inaonesha kwamba kuna kasoro ndogo zilizojitokeza katika awamu hiyo ya kwanza, ingawa pia kuna mafanikio kwa kiasi kikubwa.
Kati ya kasoro hizo ni pamoja na zilizopata kuzungumzwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji (mstaafu) Joseph Warioba, hususan madai ya kuwapo kwa baadhi ya wanasiasa, ama moja kwa moja au kupitia vyama vyao, wanaopandikiza mawazo yao yanayobeba ajenda zao za kisiasa ili wananchi wasaidie kuyapa uhalali zaidi mawazo hayo mbele ya tume ya Katiba.
Hii ni kasoro ambayo hatutarajii itajitokeza katika awamu ya pili ya ukusanyaji maoni. Hatutarajii hivyo kwa sababu tunaamini kwamba, wanasiasa ni kati ya makundi yenye nafasi ya kutoa maoni yao moja kwa moja mbele ya tume kama ilivyo kwa makundi mengine ya kijamii nchini.
Ni jambo linalotia shaka kuona baadhi ya wanasiasa au vyama vya siasa vinakwepa kutumia nafasi yao ya kutoa maoni moja kwa moja na badala yake, kufanya hivyo kupitia mlango wa nyuma, yaani kupitia midomo ya wananchi wengine ambao nao, kwa nafasi zao na mifumo yao ya kimaisha, tunataraji wanayo maoni tofauti ambayo ni muhimu katika kuelekea kuandika Katiba mpya.
Wanasiasa na vyama vya siasa ni vema wakaelewa kuwa, kazi ya tume ni kukusanya mawazo mchanganyiko kutoka kwa watu wa sekta zote. Kama alivyopata kueleza Jaji Warioba, kundi moja tu katika jamii ya Watanzania, likiwamo kundi la wanasiasa, halina si tu haki bali hata wajibu wa kumiliki mawazo ya Watanzania wengine nje ya kundi hilo.
Ni lazima tuelewane kwamba, Katiba mpya iliyotengenezwa kwa mawazo ya wanasiasa pekee haiwezi kuwa Katiba bora kwa nchi. Lakini pia tuelewane kwamba, kila kundi la kijamii nchini linayo fursa huru ya kutoa maoni, lakini fursa hiyo inalindwa kwa masharti mengine.
Miongoni mwa masharti yanayolinda fursa hiyo huru ya kutoa maoni kuhusu Katiba ni kutohodhi maoni mapya na bora zaidi kutoka kwa wananchi wengine.
Ni matarajio yetu kwamba, awamu ya pili ya kukusanya maoni haitaingiliwa na wanasiasa, ambao, ni dhahiri upeo wao umetawaliwa na swali kuu kwamba, ni kwa namna gani wanaweza kubaki madarakani au kuingia madarakani kwa mara ya kwanza.
Wito wetu ni kwamba, maoni yanayotafutwa ili kupata Katiba mpya hayalengi kusaidia chama fulani kuingia au kuondolewa madarakani.
Lengo la maoni yanayokusanywa ni kuweka mfumo mzuri wa kikatiba kwa ajili ya kujenga taifa bora, litakalomnufaisha kila raia. Busara zitawale awamu ya pili ya ukusanyaji maoni.

Comments

Popular posts from this blog