Pacha wa Mbuyu kujiunga Yanga

Yanga wakishangilia bao wakiongozwa na Hamis Kiiza na Mbuyu Twite
DORIS MALIYAGA, KIGALI
MNYARWANDA Mbuyu Twite amefuta ukimya na kuzungumzia ujio wa pacha wake katika timu ya Yanga.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Mbuyu alisema Yanga imemwahidi kumsajili pacha wake, Kabange Twite wakati wa Dirisha Dogo la usajili Novemba mwaka huu.

"Kweli Yanga waliniambia watamsajili, Kabange na nitacheza naye hapo baadaye.

"Lakini kabla ya hapo atakuja Dar es Salaam nitakuwa naye mara tu atakapotoka Congo," alieleza Mbuyu na kubainisha kuwa kwa sasa Kabange anafanya mazungumzo na Lupopo ya Congo baada ya kumalizana na APR ya Rwanda.

Mbuyu alisema licha ya kumkosa pacha wake, ambaye kwa kawaida lazima wacheza timu moja, alisema atajituma na kuhakikisha anaisaidia Yanga.

Hata hivyo, Yanga ikimchukua Kabange itafuata nyayo za Azam FC, ambayo ina mapacha Kipre Tchetche na Kipre Bolou.
Azam ilianza kumsajili Tchetche, Januari 2011 lakini ililazimika kumfuata pacha Bolou baada ya miezi sita ili ndugu hao wawe timu moja.

Hofu ya mashabiki wa Simba
Alieleza pia anafahamu atakuwa na wakati mgumu kutoka kwa mashabiki wa Simba na kuongeza hatashindwa kuifanya kazi yake kwa ufasaha akiogopa kelele za mashabiki wapinzani.

"Siwezi kuhofia mashabiki na wanatakiwa kuelewa mimi si mwenye makosa isipokuwa viongozi wao ndiyo walifanya mambo kinyume cha taratibu.

"Nitakuja Tanzania kwa ajili ya kazi na nitafanya hivyo sitakubali kucheza chini ya kiwango kwa sababu ya woga.

"Nimesajili Yanga na sasa ndiyo klabu yangu, naipenda na nitaitumikia kwa moyo wote," alifafanua Mbuyu.

Mwanasoka huyo amejiunga na Yanga baada ya vita ya kihistoria ya usajili iliyotokea mjini Kigali iliyozihusisha Simba na Yanga.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alitua mjini Kigali na kumsainisha Twite na kurudi akitamba Dar es Salaam kuwa amempiga bao Mjumbe wa Yanga, Abdalla Bin Kleb, ambaye alikuwa Rwanda pia kumwinda Twite.

Bin Kleb aliapa kuwa angelipa kisasi cha kuiliza Yanga na ndicho kilichotokea kwani alitumia mwanya wa Simba wa kumsainisha Twite pekee na kutozingatia suala la kuonana na timu yake ya Lupopo ya Congo.

Yanga ikaibuka kidedea baada ya kumalizana na Lupopo na mchezaji mwenyewe.

Twite yupo na Yanga iliyoweka kambi katika Hoteli La Pallise iliyopo eneo la Remera karibu na Kigali.

Comments

Popular posts from this blog