WACHEZAJI wa Ligi Kuu ya mpira wa kikapu Marekani (NBA), Hasheem
Thabeet na Luol Deng, wamemaliza kliniki ya siku mbili ya mchezo huo
kwa vijana jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, huku wakibainisha
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye vijana wenye vipaji.
Kliniki hiyo yenye lengo la kusaka vipaji, ilifanyika kwenye kituo cha
vijana cha Don Bosco, Upanga na kushirikisha zaidi ya vijana 200,
kutoka shule za sekondari mkoani Dar es Salaam.
Hii ilikuwa ni kambi ya mafunzo ya pili mwaka huu, chini ya udhamini
wa kinywaji cha Sprite, baada ya ile ya awali kufanyika Juni chini ya
usimamizi wa Thabeet na kushirikisha vijana chini ya miaka 17 kutoka
mikoa mbalimbali nchini.
Akichezea timu ya Oklahoma City Thunder ya Marekani, Thabeet ambaye ni
kijana wa kwanza wa Kitanzania kucheza ligi maarufu duniani ya NBA,
ameahidi kuwa, ataendelea kuunga mkono juhudi za kusaidia mpira wa
kikapu nchini, kwa kuendesha kliniki zenye lengo la kuibua vipaji na
kuuendeleza.
Thabeet aliyesoma Shule ya Sekondari Makongo jijini Dar es Salaam,
ameonesha uwezo mkubwa katika mpira wa kikapu na hivi karibu,
alisajiliwa na Oklahoma City Thunder (OKC).
Kabla ya kujiunga na OKC, Thabeet alichezea timu za Memphis Grizzlies
(NBA), Dakota Wizards (NBA D-League), Houston Rockets (NBA), Rio Grande
Valley Vipers (NBA D-League), na Portland Trail Blazers (NBA).
Kwa upande wake, nyota wa Chicago Bulls, Luol Deng, mwenye asili ya
Sudan, ambaye alishiriki michezo ya Olimpiki iliyofanyika London hivi
karibuni, alisema kuwa, amejisikia fahari kuendesha kliniki hiyo hapa
nchini.
“Hii imekuwa kliniki yenye mafanikio sana na tumeweza kubaini vipaji vingi,” alisema Deng.
Kwa upande wake, Meneja Bidhaa Msaidizi wa Coca-Cola Tanzania, Warda
Kimaro, alisema, Sprite ina furaha kusaidia mpira wa kikapu kwa vijana
hapa nchini.
“Ni imani yetu kuwa, kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Kikapu
Tanzania (TBF), tutaweza kubaini vipaji zaidi na kuendeleza mchezo huu
hapa nchini,” alisema Warda.
Naye Makamu wa Rais wa TBF, Phares Magesa, alikiri kuwa, vijana
walioshiriki kliniki hiyo, wameonesha uwezo wa hali ya juu na kuishukuru
Kampuni ya Coca-Cola kupitia kinywaji chake cha Sprite kwa kudhamini
programu za vijana, hivyo kusaidia kuibua vipaji na kuendeleza mchezo wa
mpira wa kikapu nchini.
Sprite, moja ya bidhaa za kampuni ya Coca-Cola, imekuwa ikidhamini
kliniki mbalimbali za mpira wa kikapu nchini tangu mwaka 2010.
Hii ni pamoja na shughuli mbalimbali zenye lengo la kuibua vipaji
vipya, kuleta hapa nchini timu ya mpira wa kikapu ya AND1 kutoka
Marekani kwa ajili ya michezo ya kirafiki, kupaka rangi viwanja vya
kikapu kwa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Pwani, Dodoma na
Mbeya.
|
Comments
Post a Comment