HARAKATI za baadhi ya vigogo na wapambe wao kuwania nafasi
mbalimbali za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya
zake, zimeanza kukitisha chama hicho.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho
iliyokutana Ijumaa iliyopita chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete,
imekubaliana kuyafyeka majina yote ya wagombea watakaobainika kushiriki
kwenye vitendo vya rushwa na wenye dosari mbalimbali.
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu
(NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye Nape alisema kuwa CC ilipokea
taarifa ya maendeleo ya uchaguzi ndani ya chama na kuridhishwa na
uchaguzi huo na kuagiza kila kikao husika kihakikishe haki inatendeka
hasa katika uchujaji wa majina ya wagombea.
“CC imeagiza kuendelea kukemea vitendo vya rushwa kwenye chaguzi zetu.
Na kuhakikisha kila anayebainika kujihusisha na vitendo hivyo au
mawakala wao hatua kali za kisheria zitachukuliwa,”alisema.
Aidha, CC pia inadaiwa kukubaliana kutofanya uchakachuaji wa majina ya
wagombea wanaoonekana kukubalika zaidi katika jamii kama ilivyotokea
kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Inadaiwa hoja hiyo iliungwa mkono na wajumbe wengi ambao walieleza
hofu yao kuwa endapo uchakachuaji huo utafanyika, kuna hatari ya
kupoteza wanachama muhimu, hivyo kujiweka katika hatari ya kushindwa
kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mmoja wa wajumbe waliohudhuria mkutano huo, alisema michakato ya
uchaguzi inayoendelea hivi sasa kwenye chama hicho na jumuiya zake, kwa
kiasi kikubwa imetawaliwa na makundi yanayokinzana ndani ya chama hicho.
Alidai kuwa, tishio kubwa linalokikabili chama hicho ni kuzika tofauti
za makundi mawili hasimu ndani ya CCM yanayodaiwa kuongozwa na Mbunge
wa Monduli, Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe.
Alidokeza kuwa makundi hayo yameshaanza rafu za kuandaa safu za
kufanikisha ushindi ndani ya chama ambazo pia zitawasaidia kupambana na
wapinzani kwenye uchaguzi mkuu.
Kada mwingine alidai chaguzi za chama zinazotarajia kufanyika baadae
mwaka huu, zinaweza kutoa taswira ya kufa au kuimarika kwa chama hicho
iwapo hila, chuki na fitina zitatawala.
Alisema chaguzi hizo zinaweza kuzalisha makundi mabaya zaidi kuliko
yale ya mwaka 2005 ambapo kundi la wanamtandao lililokuwa likimpigia
debe Rais Kikwete lilidaiwa kuendesha siasa chafu dhidi ya wapinzani
wao.
Miongoni mwa wapinzani walioshughulikiwa na wanamtandao ni Fredrick
Sumaye, John Malecela na Salim Ahmed Salim walionekana kutoa upinzani
mkali kwa Rais Kikwete.
Hata hivyo, baada ya CCM kumpitisha Kikwete, inadaiwa makundi hasimu
yaliendelea kukinzana, hivyo kusababisha chama na serikali kushindwa
kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Mbali na hayo CC imepinga kauli za Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Membe na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ulinzi na Usalama, Lowassa juu ya mvutano baina ya Tanzania na
Malawi.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya kikao hicho, wajumbe
walipinga hatua zozote za maandalizi ya kuingia vitani na Malawi juu ya
kugombea mipaka ya Ziwa Nyasa.
Kilidokeza kuwa, wajumbe wengi waliunga mkono kauli ya Rais Kikwete,
kuwa Tanzania haina sababu ya kuingia vitani na nchi hiyo jirani bali
wataalamu wa nchi zote mbili wapewe fursa ya kufanya mazungumzo.
Katika hilo, Nape alisema kuwa CC ilipokea taarifa ya mgogoro huo na
kuridhika na hatua zilizochukuliwa kuutatua kwa njia ya amani na hivyo
kuwatahadharisha wanasiasa na vyombo vya habari vinavyochochea vita na
uhasama kati ya nchini hizo kuacha mara moja na kuiachia diplomasia
ichukue mkondo wake.
Mwakyembe, Kagasheki wasifiwa
Katika hatua nyingine CC, imeeleza kuridhishwa na utendaji wa
mawaziri, Dk. Harrison Mwakyembe wa Ujenzi, Balozi Khamis Kagasheki wa
Maliasili na Utalii na Dk. Abdallah Kigoda wa Viwanda na Biashara katika
kuwachukulia hatua wakuu wa mashirika ya umma waliojihusisha na
ubadhirifu.
Bila kuwataja kwa majina, Nape alisema kuwa CC ilipokea taarifa ya
maendeleo ya utekelezaji wa maagizo yake juu ya kushughulikia mapungufu
yaliyooneshwa kwenye taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na kamati mbalimbali za Bunge.
“CC imeipongeza serikali kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa dhidi ya
mapungufu hayo, hasa hatua dhidi ya wakuu mbalimbali wa mashirika kadhaa
ya umma, kama vile Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), Shirika la
Viwango (TBS), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Ndege
Tanzania (ATC) na Wizara ya Maliasili na Utalii,” alisema.
Hata hivyo, licha ya kutotajwa kwa majina, mawaziri hao watatu
wameanza kazi kwa vitendo ikiwa ni kuwasimamisha kazi baadhi ya vigogo
kwenye wizara zao waliokuwa wakituhumiwa kujihusisha na ufisadi.
Dk. Mwakyembe ameanza kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa ATC, Paul Chizi na wakurugenzi wanne kutokana na ukiukwaji wa
sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma. Na wiki aliyopita
amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu TPA, Ephraim Mgawe na viongozi
wengine watatu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za ufisadi
zinazowakabili.
Waziri Kigoda yeye alianza kazi kwa kumsimamisha aliyekuwa Mkurugenzi
Mkuu wa TBS, Charles Ekelege ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi
zilizokuwa zikimkabili.
Agosti 13 mwaka huu, Waziri Kagasheki, alitangaza kuwatimua kazi
vigogo watatu wa wizara yake akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori, baada ya
kubainika kuhusika katika kashfa ya utoroshaji wanyamapori hai kupitia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda nje.
Vile vile wiki aliyopita, alitangaza kubadili utaratibu za kuwapata
wajumbe wa bodi zilizoko chini ya wizara ambapo kuanzia sasa
watapatikana kwa njia ya ushindani badala ya kuteuliwa moja kwa moja na
waziri.
Nape aliongeza kuwa, itakumbukwa kuwa CC iliagiza pamoja na viongozi
wa kisiasa kuchukuliwa hatua kwa mapungufu yale, ipo haja ya
kuwachukulia hatua watendaji wakuu wa mashirika yaliyohusishwa na
ubadhirifu mbalimbali.
“Kamati Kuu inawapongeza mawaziri husika na watendaji wote wa serikali
walioanza kutekeleza agizo hili kwani mwisho wa siku maisha bora kwa
kila Mtanzania yatawezekana,” alisema.
|
Comments
Post a Comment