KASEJA ATOKEZEA IKULU

KIGALI, RWANDA
KATIKA mazingira ya kutatanisha kipa wa Simba, Juma Kaseja aliitwa kuingia katika msafara wa Yanga uliokwenda kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame juzi Alhamisi usiku kwenye Ikulu ya nchi iliyoko mjini Kigali.

Mmoja wa walinzi wa Kagame ndiye aliyeboronga baada ya kutaja jina la kipa huyo kama miongoni mwa watu waliokuwamo kwenye msafara huo ulioongozwa na Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Fatuma Karume.
Jina la Kaseja lilifumuka wakati mlinzi huyo wakati akisoma majina ya msafara wa Yanga waliokuwa wamealikwa na Rais Kagame.

Yanga walikwenda kumwona Kagame, ambaye alitaka kuwapongeza baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame.

Sinema nzima ilianza hivi: Yanga walipofika Ikulu kulitakiwa kuwasilisha majina kamili ya wahusika wote watakaoingia ndani ikiwa ni hatua ya kudhibiti usalama kama ilivyo kawaida watu wanapotembelea sehemu nyeti kama Ikulu.

Mlinzi huyo alikuwa na orodha ya majina hayo na alikuwa akiita watu kwa sauti na kila mwenye kusikia jina lake alitakiwa kuingia ndani.

Aliita orodha hiyo kuanzia makipa halafu wachezaji wengine, lakini alivyokuwa akiendelea akataja jina la Juma hapo ndipo utata ulipozuka kwani mlinzi huyo alionekana kubabaika kusoma jina la ukoo la mchezaji husika.

Akasoma vizuri jina la Juma lakini akaona isiwe taabu akaamua kumalizia kwa kutamka Kaseja na kuwafanya watu wa Yanga kushikwa na butwaa.
"Juma... Juma...Ka..se.ja" aliita mlinzi huyo kwa kubabaika
Hata hivyo, Mwanaspoti iligundua kuwa mlinzi huyo alitatizwa na jina la Juma Seif Kijiko na badala yake akasoma Juma Kaseja.

Hata hivyo, pengine mlinzi huyo alikuwa na kumbukumbu ya Kaseja kwani aliwahi kuchezea timu hiyo katika msimu wa 2008/2009.

Si siri pia Kaseja ni maarufu katika medani ya soka ya nchi za Afrika Mashariki na Kati kwani ameng'ara na Simba na Taifa Stars kuanzia mwaka 2002 katika mashindano ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanzia yale ya klabu na timu za taifa.

Comments

Popular posts from this blog